day, June 12, 2012
BASATA: WASANII JIPANGENI KUHIMILI USHINDANI WA KIMATAIFA
Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujipanga kwa ajili ya kuhimili ushindani wa
kimataifa kutokana na ujio wa mfumo wa digitali ambao utazifanya kazi zao
kuonekana kimataifa.
Wito huo umetolewa
wiki hii kwenye ukumbi wa BASATA na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ghonche
Materego wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa uliohusu Teknolojia
ya Digital na Faida Zake Katika Sekta ya Sanaa uliochokozwa na Mhandisi
Joel Chacha kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Tcra).
Alisema kuwa, mfumo
wa digitali utaruhusu uwepo wa vituo vingi vya redio na runinga ambavyo
vitakuwa na masafa ya kimataifa hivyo ni wazi wasanii wanatakiwa kujipanga
katika kuandaa maudhui bora, ya kutosha na yenye mvuto kwa ajili ya kukidhi
ongezeko hilo na zaidi ushindani wa kimataifa.
“Wasanii tujipange,
fursa zinazokuja ni nyingi mno, zinahitaji maudhui ya kutosha, yenye ubora na
yatakayoweza kuvifanya vyombo vya habari viweze kuhimili ushindani pia”
alisisitiza Materego.
Aliongeza kuwa,
moja ya eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wamiliki wa vyombo vya habari ni
uhafifu wa maudhui ya kazi za Sanaa hivyo, wasanii hawana budi kuacha
kulalamika na kujipanga kukabili changamoto hiyo.
Awali akiwasilisha
mada hiyo,Mhandisi Chacha alisema kuwa, mfumo wa digitali utazalisha fursa
nyingi katika sekta ya Sanaa lakini akasisitiza kuwa, uchangamfu wa Wasanii
wetu ndiyo utawafanya wafaidi.
Alizitaja baadhi ya
fursa hizo kuwa ni pamoja na; ongezeko la ajira kwa Wasanii, ongezeko la
vipindi, kukua kwa ushindani katika ubunifu na utengenezaji maudhui yenye
ubora, Sanaa za Tanzania kutangazika kimataifa na kuongezeka kwa makampuni
yatakayojihusisha na sekta ya Sanaa
“Mfumo wa digitali
una mazuri mengi lakini kubwa ni kuongezeka ushindani na ubora katika
kutengeneza maudhui yenye ubora na pia ongezeko la masafa katika televisheni
ambayo yatahitaji maudhui (vipindi) ya kutosha” Aliongeza Chacha.
Hata hivyo,
aliitaja changamoto ya uharamia kwenye sekta ya Sanaa ambapo aliwashaiuri
wasanii kuamka na kujiunga na Chama cha hakimiliki (Cosota) ili kuhakikisha
kazi zao zinalindwa kisheria.
Wadau wengi
waliochangia mjadala huo walionekana kuwa na wasiwasi na mfumo wa digitali
lakini wakaomba elimu ya kutosha itolewe ili wananchi wengi zaidi waelewe nini
maana ya kutoka mfumo wa analogia kwenga ule wa digitali.
No comments:
Post a Comment