Tuesday, June 12, 2012

IDARA YA HABARI NA WASEMAJI WA WIZARA, TAASISI NA HALMASHAURI ZA WILAYA NA MIKOA WATAKIWA KUJIPANGA KATIKA KUISEMEA SERIKALI


  IDARA ya Habari ( MAELEZO) imetakiwa kujipanga  vizuri ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya kuwa Msemaji wa    Serikali ipasavyo; hatua hiyo itasaidia kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na utendaji wa Serikali.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali katika ukumbi wa Victoria Palace Jijini Mwanza.
Aidha, Dkt. Mukangara alisema, Idara ya Habari ( MAELEZO) ina jukumu zito la kuwa Msemaji  Mkuu wa Serikali . Hii ni kwa mujibu wa agizo la Serikali Na. C 16 la mwaka  1977.
" Serikali inafanya mambo mengi  mazuri kwa wananchi lakini hayasemwi. Matokeo yake Serikali inaishia kulaumiwa na wananchi bila sababu.
"Ndugu zangu hali hii haikubaliki. Lazima tubadilike na lazima tuseme . Hatuwezi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali asiyesema." Alisema Dkt. Mukangara.
Dkt. Mukangara aliongeza kuwa Idara ya habari itekeleze jukumu hilo kwa kushirikiana na Wasemaji wa Wizara na Taasisi mbalimbali  za Serikali na Wasemaji hao watambue kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ni Idara ya Habari.
Akizungumzia  kuhusu uhuru wa vyombo vya habari alisema,tunalo tatizo la baadhi ya vyombo vya habari  nchini kudhani kwamba uhuru wa vyombo vya habari hauna mipaka. Hivyo alivitaka vyombo vya  habari vitambue kuwa hakuna nchi yoyote duniani ambayo utendaji wa vyombo vyake vya habri haubna mipaka.
" Wakati wote uhuru wa vyombo vya habari  popote pale huendana na wajibu hata ktika mataifa yaliyoendelea"Alisema Dkt. Mukangara.
Aidha, alivitaka vyombo vya habari kuwa makini katika kutangaza habari zinazohusu mchakato wa mabadiliko ya katiba huku akisissitiza kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kuwahabarisha wananchi na kutoa elimu.

 
Dkt. Mukangara pia aliwataka Maafisa  hao kuhakikisha kwamba wanaelimisha wananchi  juu ya umuhimu wa zoezi la Sensa ya watu na Makazi.
Baadhi ya mada zitakazojadiliwa katika kikao hicho cha siku tano chini ya Uenyekiti wa  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Sethi Kamuhanda, ni pamoja na Changamoto za utaratibu wa usajili wa magazet; Changamoto zinazoikabili Tanzania katika kuhama  kutoka Analojia kwenda Digitali kufikia mwaka 2012; Wajibu wa Maafisa Mawasiliano na mfumo wa mawasiliano Serikalini; na  Kazi za Serikali Mtandao na Tovuti kuu.
Kwa upande wake Afisa Habari  wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Bi Monica Mutoni  alisema kikao kazi hiki ni fursa kwa Maafisa Habari kuboresha kazi zao  na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwahabarisha wananchi majukumu ya Serikali.
Naye Afisa Habari wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Bw. Leonidas Tibanga alisema kuwa baada ya kikao kazi hicho,  Maafisa Habari wataweza kupata ujuzi mpya kutokana na mada zitakazotolewa, na kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa mawasiliano miongoni mwao.
Vikao kazi vya Maafisa Habari vimekuwa vikifanyika kila mwaka  chini ya uratibu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamduni na Michezo ili kujadili namna bora ya utoaji habari za Serikali na uimarishaji wa mawasiliano kwa umma

No comments:

Post a Comment