Monday, December 17, 2012
Kwanini watu huogopa maiti, makaburi, chumba na nguo za marehemu? Wanawake na watoto wanaongoza Mawe yana maana gani juu ya kaburi?
Na Cosmas J.Pahala
WATU wengi huogopa kupita katika maeneo ya mskaburi hususan nyakati za usiku. Wengine wakiogopa kulala chumba chenye maiti au hata mahali ambapo mtu fulani alifia.
Robi Mashauri na Mdogo wake Shida (20) wa Sabasaba Tarime, walikataa katakata kuingia katika chumba chao kwa kuwa mwili wa mmoja wa wapangaji wao, Mariamu Nyangarya, aliyefariki kutokana na ujauzito katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, ulikuwa katika mojawapo ya vyumba vya nyumba wanayoishi.
Kila walipotaka kuingia ndani, walilazimika kukusanyana na wadogo zao, wakawasha taa na kuingia kwa pamoja wakiwa kundi kubwa.
Philotea Temu (26), mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, anasema, ‘Baba alipofariki tulipeleka maiti nyumbani kwetu huko Moshi kwa mazishi, lakini sisi tulitangulia kurudi ili tuendelee na masomo na mambo mengine ya nyumbani.’ ‘mama alituagiza tukifika nyumbani, tutoe vitu vyote kwenye chumba cha marehemu baba ili tufanye usafi, lakini tulipofika huku nyumbani (Dar), wote ; mimi na ndugu zangu watatu tulibaki kutupiana ingia wewe ; ingia wewe na mwishowe, wote tukataa kabisa hadi mama aliporudi baada ya wiki.’
Anaongeza, ‘Unajua kama mimi huwa ninajihisi kuwa labda nitakutana na marehemu huko ndani na kwamba huenda alikuwa ananipenda sana hivyo, atataka tukae nae pamoja, hapo ndani, au atataka twende naye katika makao yake mapya na ya milele.’
Kwa mujibu wa mmoja wa vyanzo vyetu vya habari ambaye hakutaka jina lake litajwe, kaka yao alipofariki dunia mwezi Julai mwaka huu, ndugu wengine walikubali kurithi chochote cha kaka yao walichopangiwa lakini mmoja wa ndugu zao ambaye ni wa kiume, aligoma kabisa kupokea shati na suruali zilizokuwa sehemu ya urithi wake, kwa mujibu wa kabila la Wakabwa.
Anasema hata baada ya wazee kuingilia kwa nguvu na kumuonya kuwa alikuwa anavunja mila kwa kuwa kitu cha marehemu hakikataliwi kupokewa na kwamba jamii ingemtazama kama aliyefurahi ndugu yao kufariki ili baadaye alirithi vitu vya thamani, alipokea, lakini baada ya muda mfupi kuwa na mavazi hayo bila kuyavaa, vitu hivyo havikuonekana tena wala hakuwa tayari kufafanua kwa yeyote kuwa vilikwenda wapi.
Wao waliofikiri kuwa labda aliuza ili kuganga njaa na wengine, walifikiri kuwa ametupa mradi tu, hakuna aliyekuwa na uhakika bwana huyo kapeleka wapi nguo hizo.
Hii tuliyoitaja, ni baadhi tu ya mifano kwani ni wazi kuwa baadhi ya watu hushindwa kulala peke yao baada ya kuona maiti.
Uchunguzi uliofanywa na KIONGOZI kwa nyakati tofauti katika misiba minane jijini Dar es Salaam hususan wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa marehemu, ulibaini kuwa wanawake watatu hadi wanne kati ya wanane, wanaopita mbele ya marehemu kutoa heshima za mwisho, hukwepa kuangalia sura ya marehemu huku wakiangali chini ama pembeni .
Ukabaini kuwa wanaume wanne hadi sita, kati ya wanane wanaopita mbele ya mwili wa marehemu kwa heshima za mwisho, humudu kuiangalia sura ya marehemu japo kwa muda mfupi huku uchunguzi huo ukibaini kuwa, wanaume wawili tu, kati ya hao wanane, hupita wakiwa wameangalia chini au bila kupinda kuangalia mwili wa maremu.
Hii ina maana kuwa hupita wakiwa wameangalia mbele.
Uchunguzi huo usio rasmi, ukabaini kuwa watoto kati ya miaka mitatu hadi mitano hivi, huwa hawaogopi kupita mbele ya marehemu, bali huogopa macho na mkusanyiko wa watu hivyo, wengine hukataa.
Hata hivyo, ukagundua kuwa wanapoona maiti na kisha mazishi yakafanywa, ndipo hutambua kuwa wamempoteza mpendwa wao.
Wengi hujikuta wakiwa na upweke mkali kwa vipindi kadha wanavyowakumbuka marehmu na kisha wakifarijiwa kwa namna fulani, ni wepesi kusahau tena.
Iligundulika katika uchunguzi huo kuwa, watoto zaidi ya mika mitano na chini ya 12, huogopa zaidi kuona mwili wa marehemu ingawa wengine hupenda kuona ili wapate namna ya kusimulia watakapokutana na watoto wenzao.
Na hao, sio rahisi kupita katika maeneo ya makaburi peke yao. Wengi, huamini kuwa nyakati za jioni au usiku, mizimu na mshetani mbalimbali hutembelea maeneo ya makaburi na wafu wengine, kutoka na kukaa juu ya mawe yaliyojengewa makaburi hayo.
Kwa ufupi, uchunguzi huo usio rasmi ulibainisha kuwa watoto huongoza kwa kuogopa wafu wakifuatiwa na wanawake, bila kujali umri.
Afisa nayeshughulikia mambo ya uhamiaji katika baraza la maaskofu Katoliki tanzania TEC, Bw. Steven Msowoya, yeye anasema, ‘Nimeona na kusikia wengine wakisema mimi sipiti hapo au siwezi kuingia humo alimokuwa maiti. Wanadai wanakuwa kama wanamuona marehemu akiwa hai na akiwatokea machoni. Hali hii inategemea zaidi umri na malezi aliyokulia mtoto.
Kama amekulia katika malezi ya kuogopaogopa vitu, inamuwia vigumu sana na ndiyo maana wengine hasa wasichana naweza kumtishia kwa jongoo akakimbia na kulia sana, lakini wengine ni shupavu kutokana na malezi aliyokulia, unaweza kumuona mtoto wa miaka kumi akipambana hadi kumuuua nyoka.’
Msowoya anaongeza, "Pengine wanaokuwa waoga sana, huenda mama zao wakati wakiwa wajawazito, walikuwa waoga, hivyo wakawarithisha uoga tangu tumboni mwao.’
Hata hivyo, kwa sababu za kisaikolojia, si vema kuwashirikisha watoto wadogo kuona au kuugusa mwili wa marehemu maana kumbukumbu hiyo itadumu kichwani . Lakini, licha ya maelezo yote hayo, hebu muulize yeyote kati ya watu wenye woga huo kwamba, huwa anaogopa nini hasa.
Ni dhahiri hakuna anayeweza kukueleza sababu inayoingia akilini.
Dk. Dafrossa Lyimo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Ilala, jijini Dar es Salaam, anasema, hali ya kuogopa maiti, makaburi vyumba na baadhi ya vitu vya marehemu, inatokana na hisia za kibinafsi na ukaribu wa kinasaba uliopo baina ya mtu huyo na marehemu.
‘Jambo hili linahitaji wataalamu wa mambo ya kisaikolojia, kwa sababu kila mtu anahisia zake na ndio maana hata madaktari, wapo wengine wanaoogopa kumpasua chura, lakini wanaweza kumpasua binadamu bila tatizo,’ alisema.
Akaongeza, ‘ …Hii haiwapati watu wote maana wengine wanaweza kufiwa, wakafumba macho na mdomo wa maiti na pengine hata kubeba wenyewe ndiyo maana nasema inategemea pia, uzoefu katika mambo kama hayo. Mfano, walioshuhudia mauaji ya Rwanda na Burundi, ataogopa maiti ?’
Naye Dk. Nargis Simmons, Mtaalamu wa Mambo ya Kisaikolojia, katika Kituo cha Mental Health Resource Center, kilichopo ndani ya eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema hali ya kuogopa mazingira yoyote ya kifo, inatokana na hisia alizokuwa nazo mtu tangu akiwa kadogo hasa kama akiwa mdogo alikuwa anatishiwa juu ya mambo ya vifo.
Dk. Nargis anasema, mila zilizopo katika jamii, zinachangia mtu kukua akiwa na fikra fulani kichwani, kuwa kama hili likiwa hivi, hili linaweza kutokea na hii mara nyingi ilikuwa ni mbinu iliyotumika katika jamii kuzuia baadhi ya mambo ambayo hayakutakiwa hivyo, fikra hiyo ikarithiwa toka kizazi hadi kizazi.
Hata hivyo, mwanasaikolojia huyo, alisema hajawahi kuona utafiti maalumu juu ya sababu hasa za watu kuogopa kifo na mazingira yanayoendana na msiba.
‘Wengine walikuwa wakisimuliwa au kutishiwa wakiwa watoto kuwa ukifanya hivi, wafu watakutokea na kukuchukua, hivyo wazo hilo la hofu linakuwa gumu kubanduka kichwani, na inapotokea msiba, basi anakumbuka na kupatwa na hali hiyo ya woga, ‘ alisema.
Akaongeza, ‘Jamii nyingine zimekuwa zikiwatishia watoto kuwa ukiongopa, wafu watakuja kukuchukua, sasa anakumbuka akilini pengine hata bila yeye mwenyewe kujijua kuwa, aliwahi kuongopa, hapo ndipo hofu humpata.’
Akatoa mfano zaidi kuwa, ‘Makabila mengine yana mila kuwa mtu mzima kama baba yako akifariki, lazima umzike kijijini ; wanasema ukimzika mjini, mizimu itachukia na kukufanya vibaya, wanaweza kusema usipofanya hivyo, marehemu baba (ndugu) yako, utakujia. Sasa, hata akilazimika kumzika sehemu nyingine, halafu likatokea tatizo la kawaida tu, anakumbuka kuwa alivunja miiko kwa kumzika baba yake mjini badala ya kijijini kwao. Hofu hiyo hivyo anairithisha kwa jamii nyingine inayomzunguka kupita masimulizi na mazungumzo’
Kitabu cha CORE PSYCHIATRY, kilichaoandikwa na James V Lucey, Uk.201, kinasema, kuwa kibailojia, sababu za hofu hizo hazijulikani.
Hata hivyo, woga huo basi ndio ulio asili ya watu kuweka mawe makaburini. Lakini je, ilianzaje ?
Katika jamii zenye utamaduni huo yakiwemo maeneo ya Mashariki ya Kati watu waliweka mawe katika makaburi wakihofu kuwa wafu wangeweza kutoka humo hata baada ya kuzikwa na kuleta madhara kwa walio hai. Hivyo, wakijaribu kujihakikishia usalama wao, ndipo walipoamua kuweka mawe mazito katika lango la kaburi ambalo waliamini kuwa, marehemu hawezi kulisogeza na kutoka.
Ukiuliza juu ya lini utamaduni huu ulianza, jibu litakuwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita kwani kule kuwekwa jiwe kubwa katika mlango wa kaburi la Yesu Kristo, nje ya mji wa Yerusalemu katika Kilima cha Golgotha, kunathibitisha hivyo.
Mwanzoni, watu walizikiwa popote; mara nyingi katika au karibu na maeneo walikofia au kuuawa.
Makaburi yalizagaa hata katika maeneo ambayo leo hii usingewazia yawepo.
Baadhi ya watu wa kale waliona maiti kama kitu cha kutisha mno, kiasi kwamba kuigusa au hata kupita eneo lenye kaburi kwao ilikuwa kama nuksi.
Kwa sababu hiyo, waliyatia makaburi alama kwa kuweka mawe ili yaonekane na kutambuliwa mapema na mpita njia.
Hiyo, ilifanywa kama alama ya onyo kwa wapitaji wasije wakasogelea kile walichoamini kuwa kinaweza kuwa balaa lingine kwa jamii.
Pia, ili kuyafanya mawe hayo ya tahadhari yaonekane kwa uwazi zaidi, mara nyingi yalipakwa chokaa.
Hatimaye wazo la kuweka makaburi katika eneo moja lilianza na ndipo maeneo maalum yaliyo mbali na makazi ya watu yakatengwa kwa maana ile ile ya kuwaweka wafu mbali na walio hai kwa ajili ya usalama.
Katika hatua juu ya kukua kwa woga wa walio hai kwa wafu, pole pole mtindo wa kuyaabudu makaburi ulianza.
Jiwe juu ya kaburi liliwakilisha nguvu za kiungu au za mzimu wa aliyeabudiwa na hii huenda ndiyo inayotumika kama njia ya kuwaomba radhi marehemu ili wasifanye mabaya katika jamii.
Katika wakati huo, watu hawakuhofia tena sana makaburini, bali waliweka mawe makubwa ili kuzuia wanyama wasiyaharibu makaburi hayo na kufukua miili ya marehemu.
Maelezo juu ya mawe ya makaburini ni jambo lililofuata baadaye kuonesha vyeo na hadhi ya marehemu na hivyo, kuwafanya wapita njia waziombea roho za marehemu hao.
Wengi wetu tumekuwa tukisoma tu juu ya kuwekwa huko kwa jiwe kaburini, lakini hatujui utamaduni huu wa kuweka mawe kaburini ulitoka wapi.
Hebu sasa tuangalie machache kuhusiana na utamaduni na sababu za kijiografia za matumizi ya mawe na mimea juu ya kaburi.
Kwa mujibu wa masimulizi, wakati Mtoto wa Adamu, Abel, alipomuua mdogo wake, Kaini, hakujua amfanyeje zaidi wala ampeleke wapi.
Kama ishara ya kumuongoza la kufanya, wakatokea kunguru wawili wakipigana, mmoja alipofariki, kunguru mmoja alichimba chini kwa kucha zake na kisha kumfukia kunguru aliyefariki.
Baadaye, kunguru yule mzima akatumia mdomo wake kuchukua kijiti na kukichomeka alipofukia.
Huo ukawa mwanzo wa kukumbuka sehemu kilichowekwa kitu kilichokufa ili pasisahaulike.
Lakini, huko Mashariki ya Kati, kulikuwa na mchanga mwingi hivyo, mvua iliponyesha, uliondoka kirahisi na hata kutokana na upepo, iliwezekana kabisa kuwapo shimo.
Inaelezwa kuwa, kutokana na mabadiliko hayo ya kijiografia, ndipo ikajitokeza haja ya kuweka mawe kwani hayakuwa rahisi kuhamishwa na maji ya kawaida au upepo.
Baadaye, kadiri maendeleo yalivyozidi, ndipo watu wakaanza kujenga makaburi kwa kutumia saluji, kuandika majina na hata kuweka alama kama msalaba ili kutofautisha dini.
Hata hivyo, bado mawe yana maana tofauti hadi sasa toka jamii moja hadi nyingine.
Mfano, kwa Kabila la Wasukuma, mawe huwekwa katika kaburi la mtu aliyeacha uzao yaani aliyeacha watoto watakaoendeleza ukoo wake.
Aidha, mimea inayostahimili ukame kama minyaa, kupandwa kaburini huashiria umilele wa kukumbukwa kwa marehemu.
Hata hivyo, ni vema kutambua kuwa, mtu akisha kufa, amekufa; amekwenda moja kwa moja; ameitwa na Mungu.
Imani za kuogopa makaburi, maiti na hata mali halali za marehemu kwa imani zisizo za kitaalamu hazina maana.
Ni vema jamii itambue kuwa imani hizo zinaweza kutumiwa na wachache wakiwamo matapeli na walaghai wanaopiga ramli ili kuwaibia watu pesa zao.
Vitu kama mawe au mimea katika ulimwengu wa sasa, hutumika kuepusha usahaulifu wa mahali kaburi lilipo endapo litakaa muda mrefu huku likinyeshewa mvua na kuwapo uwezekano wa kutawanyika.
Ujenzi wa makaburi na matumizi ya mawe na mimea ni kumbukumbu ya jamii kwa ndugu yao aliyefariki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment