Monday, December 17, 2012
Wakurya: Kuwatahiri wanawake kwa siri ni kujikomoa wenyewe Wajawazito hutahiriwa wakati wa kujifungua Watoto wachanga wanapozaliwa je nini hutokea?
Na Cosmas J.Pahalah
KIJANA! Njoo utazame vyumba vipo viwili, sasa wewe chagua unachopenda, ulipie kwa miezi sita au mwaka mzima; uhamie hata leo,” akasema Mzee mmoja eneo la Kurasini, Dar es Salaam Samweli Matiko, alilipofika kwake kutafuta chumba kwa ajili ya kuanza maisha yangu.
Matiko alifurahi mno na hata akaridhika na chumba huku akiwa tayari kulipia kwa msimu mzima wa mwaka. Balozi katika shina lile akaitwa kushuhudia kutiliana saini katika mkataba ule wa kupanga katika nyumba hiyo yenye uzio mzuri na wapangaji wengine mchanganyiko, wa kike na wa kiume.
Huku kikao! hicho kikiwa katika mtindo wa mzunguko, mmoja wa wajumbe wa kikao kile akataka wazidi kujuana zaidi maana binadamu bwana, pengine hata labda wale ni ndugu wasiojuana.
Akarudia tena, “Ninaitwa Samweli Matiko.” Akauliza zaidi, “Mwenyeji wa mkoa gani?” “Mimi mwenyeji wa Musoma mae…”. Ghafla, Baba mwenye nyumba akadakiza kwa mshituko, “Wewe ni mtu wa Musoma? Ni Mkurya?” Matiko akawahi kuitikia kwa ufahari, “Ndiyo mimi mtu wa Musoma na ni Mkurya kabisa vipi na wewe ni mtu wa huko nini?”.
“Sikia kijana kama wewe ni Mkurya (akiwa na maana ya Mkoa wa Mara), afadhali nimejua kabisa. Utanisamehe nyumba yangu sipangishi Mkurya. Siwezi! Siwezi kijana utanisamehe; samahani kwa kuwasumbua.,” akasema huku akininyooshea mkono kunirudishia pesa aliyokuwa nayo tayari mkononi mwake.
Kibaya zaidi, kadiri Matiko alivyozidi kumsihi Mzee yule ampe chumba, ndivyo Mzee alivyozidi kuwa mkali. Matiko akafyata mkia na wapambe wake aliokuwa nao.
“Twende bwana mimi siwezi kuficha kabila langu,” akasema huku wakiondoka pale.
Wakaendelea na juhudi za kutafuta chumba mahali pengine huku wakitoa tenda kwa watafuta vyumba maarufu mtaani wanaoitwa madalali.
Hazikupita siku tatu, dalali akafika akimtafuta pale alipokuwa anaishi. kwa hifadhi “Mali (chumba) imepatikana sasa ulaze damu mwenyewe.” Wakaenda jioni hiyo.
Wakamkuta mama mwenye nyumba hapo Kekomachungwa. wakasalimia na kisha yule dalali akamwambia mama yule, “Mama huyu ndiye mgeni wako.”
“Baba wewe mtu wa wapi?” “Kwetu ni Musoma. Baba ni Mkurya na mama ni Mkurya.”
Mama akaguna kidogo na kusema, “Umeishapata mwenzako baba (akimaanisha kama Matiko ameoa). Akamjibu, “Kwa kweli bado ; ndio ninaanza maisha sasa.”
“Bahati mbaya mwanangu.” “Kwanini unasema hivyo?” Matiko akasaili ili kujua kulikoni tena. “Ni bahati mbaya kwa sababu kwanza sipangishi kijana ambaye hajaoa au ambaye hajaolewa. Hilo ni moja, la pili, siwezi kukaa na Wakurya wala binti wangu hawezi kuolewa na Wakurya.”
Sasa Matiko akachanganyikiwa maana aliyeumwa na nyoka, hata akiguswa na nyasi anashituka.
Safari hii hakutaka ubishi wala kubembeleza. akaaga wakaondoka.
Njiani kila mmoja wetu alikuwa na lake alililojiuliza.
“Kumbe ndiyo maana siku hizi sio jambo geni kumsikia kijana yeyote hata akiwa mtaani akijitambulisha kwa watu kuwa ni mtu wa kabila lingine (si Mkurya au hatoki mkoani Mara)!” Mmoja akasema kwa sauti.
Mambo haya yakamchanganya sana Matiko maana kwa kiasi kikubwa, jambo la ukabila hutokea hasa kwa vijana wanaotafuta vyumba vya kupanga au wale wanaochumbia au kuchumbiwa.
Sasa sababu za vijana hao kuficha kabila lao zikaanza kubainika. Ikabainika siri iliyofichika sirini.
Mara nyingi unapojitambulisha katika jamii kuwa wewe ni Mkurya, uwe na uhakika kuwa huenda lengo lako litaishia patupu kwa kukatalaiwa kila unapoenda .
Hii ni kwa sababu kuna dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa Wakurya ni wakorofi, wagomvi na mengine mengi ya namna hiyo.
Kwa mazingira na uelewa wa kawaida, dhana hiyo inaweza kweli ikawa sahihi au isiwe sahihi kwani, wote wanaopiga au kuua wake zao ni Wakurya?
Ni vigumu kuafiki moja kwa moja dhana ya jumla kuwa Wakurya ni wakorofi kwani ninajua kuwa tabia ya mtu licha ya kutegemea mazingira ya malezi aliyozaliwa na kulelewa, bado inategemea mtu mwenyewe.
Hata hivyo, ukweli unabaki palepale kuwa mila na desturi za kabila hilo, zinakuwa kichocheo kikubwa katika dhana hii. Ugomvi wa namna zote pamoja na unyanyasaji wa wanawake, ni vitendo vilivyokithiri na hata kuwa tishio kwa makabila mengine.
Inasikitisha kwa ndugu zetu Wakurya wameulinganisha na kuuchukulia ugomvi kuwa kama moja ya mahitaji yao muhimu.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vitu vya kawaida kusikika masikioni mwa watu na ni dhahiri kuwa, kama Serikali isingeamua kuingilia kati, sijui jamii ya Wakurya ingekuwa na tofauti gani na Wahutu na Watutsi.
Kinachosikitisha hapa ni kwamba, badala ya Wakurya kuutambua upendo wa Kimungu kama ndugu, bado majaribio ya kumwagiana damu yanajirudia miongoni mwao.
Hivi hata katika mwanzo huu wa miaka ya 2000, ambao dunia imo katika Karne mpya, bado Wakurya wanataka kubaki katika zama zile za miaka ya huko kisogoni?
Hivi kimantiki, kwanini Walenchoka na Wanchali wapigane na kumwagiana damu, kusababishiana vilema na kugeuzana wakimbizi? Kama ilivyokuwa nyuma, kwanini Wakira na Wanyabasi wapigane ? Uadui unatoka wapi wakati wote ni familia moja ya Wakurya ndani ya nyumba moja ya Tanzania?
Tukiachana na vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe, miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya wanaume kufanya ukatili dhidi ya wanawake.
Mfano, mwaka 1999, huko Ronsoti wilayani Tarime, Bw. Turia Nyakemu, alimgecha (kumkata mtu kwa panga) mithili ya mti wa porini, mkewe, Ester Turia eti kwa madai kuwa, akizaa watoto wanakufa (kwa sasa hatujui hatima ya shauri hilo).
Hivi kama sio unyanyasaji unaoogopesha hata makabila mengine, alipimwa na nani hata ikabainika kuwa tatizo la Ester kutozaa lilitokana na yeye na wala si mwanaume au vinginevyo?
Hivi mwanamke kama alivyo, anaweza kuzuia watoto wasife?
Pia, katika Kijiji cha Borenga wilayani Serengeti, Bw. Mwikwabe Ryoba, aliwahi kufungwa na kukalizwa juu ya moto ulioandaliwa kwa makusudi eti akituhumiwa kufanya mapenzi na mke wa jirani yake.
Labda jambo muhimu la kujiuliza hususan kwa jamii ya sasa ya Wakurya ni kwamba, mtindo huo wa maisha wa kujichukulia sheria mkononi, bado uko kwenye fasheni hadi sasa au la?
Hivi tukiwa wakweli, ni nani asiyejua ukweli juu ya adhabu kali wanazopewa wanawake wa Kikurya toka kwa waume zao? Ni wangapi tumewasikia kuwa wamechomwa hata sehemu nyeti na waume zao?
Tunajua avumaye baharini ni papa, lakini na wengine wapo, lakini ukweli ni kwamba, licha ya kuwa madhambi hayo sasa yanafanywa hata na makabila mengine yakiwamo ya mikoa ya Kusini mwa Tanzania, bado hapa ninajadili Wakurya kwa sababu ndio jina lao limeenea sifa hiyo mbaya.
Mfano, hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania ilipokutana wilayani Tarime, iliwatia hatiani baadhi ya watu kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya mauaji.
Mahakama hiyo ilimhukumu Oranda Nyakua (35), mkazi wa Utegi, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Pamela Nyakua, kwa kumgecha mapanga.
Tukio hilo lilidaiwa kutendeka Oktoba 11, 1995 katika kijiji cha Masike wilayani Tarime.
Septemba 30, mwaka huu, Mahakama Kuu hiyo, ikamtia hatiani na kumpa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, mkazi mmoja wa Kijiji cha Tagota wilayani Tarime, Lucas Kimito(69), kwa kosa l;a kumuua mkewe Wegesa Kimito.
Ilidaiwa kuwa, tukio hilo lilitokea Machi 12, 1995, baada ya Bw. Kimito kumshambulia kwa ngumi na ufagio hadi kumuua mkewe kutokana na ugomvi wa kifamilia.
Ninajua dhahiri kama nilivyotangulia kusema kuwa, unyanyasaji wa namna hiyo unatokea kabisa hata kwa makabila mengine, ila kinachonisikitisha, ni kukithiri kwa kwa unyanyasaji huo ndani ya Wakurya.
Hivi ni kweli kuwa licha ya umuhimu wa mwanamke yeyote kujulikana kwa kiasi kikubwa namna hii ndani ya jamii, bado Mtanzania mwenzako mwenye majukumu mengi namna hii, ananyanyaswa kwa ukatili wa makusudi; Tanzania ya kesho italindwa na kujengwa na nani?
Tukiachilia mbali unyanyasaji huo unaomfanya mwanadamu aonekane mnyama kuliko mnyama halisi kwa njia ya vita, hebu sasa tuutazame huu unaofanyika kwa kisingizio cha mila na desturi.
Ninajua zipo mila nyingine nzuri ambazo hazina budi kuigwa na kuboreshwa ili ziendelee zaidi, pia zipo ambazo kwa udi na uvumba hazina budi kuachwa kabisa kwani zimepitwa na wakati na zina madhara makubwa katika jamii kiroho na kimwili.
Ni kweli kuwa unapofikia umri wa ujana; kijana wa Kikurya hupelekwa jandoni ambako hufanyiwa tohara hali inayoonesha kuwa yuko tayari kuoa au kuolewa na kuwa baba au mama safi wa familia; hivyo kipindi hiki ni muhimu sana kwani ni huko wanapoadilishwa namna ya kuishi vema.
Hata hivyo kipindi cha jando kimekuwa na umuhimu mkubwa kwani hapo vijana wanafunzwa na kuchochewa moyo wa ari na ujasiri. Pia kupitia jando na tohara kwa vijana, kumekuwepo na heshima kati ya rika moja na nyingine maana pamoja na umri, bado rika iliyotanguliwa kutahiriwa (kwa Kikurya huitwa Esaro), huweza kuheshimika sawa na baba au mama maana hata makamo yao huranda.
Tofauti na hali ilivyo sasa kuwa mzee anayelingana na baba anaweza kumtania binti mdogo sawa na mwanae kama nionavyo mijini na hata wanataka ‘kujenga mazoea ya karibu’ hilo katika jamii ya Wakruya halifanyiki kutokana na msaada wa rika ya jando.
Kwa wenzetu hawa wenyeji wa Mkoa wa Mara, hususani Tarime Musoma-Vijijini na Bunda, mvulana ambaye hajatahiriwa (Umurisya), msichana (Omosaghane) na mwanamke aliyezaa kabla ya kutahiriwa (Irikunene) ni watu wanaochukuliwa na jamii kama watoto wadogo na hawana sauti ndani ya jamii. Kufanya mapenzi nao ni aibu, dhambi na kashfa.
Katika makala haya ya leo ugomvi haupo katika neno tohara, bali TOHARA KWA WANAWAKE licha ya juhudi za Serikali na wataalamu wa afya kubainisha athari zote za tohara kwa wanawake ikiwa ni pamoja na kupelekea vifo wakati wa kujifungua, kuvuja damu baada ya kitendo hicho na pengine kupotezaa maisha, bado Wakurya wanayo ile dhana kuwa kitendo hicho ni sawa na Speed Governer yaani hupunguza taama za kimwili kwa wanawake.
Ni kutokana na imani hiyo ambapo licha ya juhudi za Serikali, vikundi vya afya, pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), kuuelimisha umma madhara hayo, na kwa kuwa Serikali imetangaza bayana vita dhidi ya unyanyasaji huu wa wanawake, unaofanywa hata na Wagogo, Wapare na Wachaga, na wenyeji wa Mkoa wa Singida, wenzetu Wakurya sasa wameamua kufanya madhambi hayo kwa kificho.
Kwa ndugu zetu Wakurya, kwa miaka ya hivi karibuni na pasi na shaka mtindo huu bado unaendelea, wamekuwa na tabia ya kumfanyia tohara Mtoto wa kike ndani ya nyumba na kufungiwa humo hadi atakapopona ili kukwepa ‘jicho’ na ‘mkono wa Serikali’ yaani kwa siri.
Si hivyo tu, bali pia saa kwa mwanamke mjamzito ambaye hajatahiriwa (Irikunene) ili kukwepa kubumbuluka kwa siri hizo, sasa kwa Wakurya na kungwi huandaliwa mpango maalumu wa siri ambapo pasipo yeye mjamzito kujua, tena wakati ule wa kujifungua, ndio huwa nafasi ya kuwafanyia wanawake tohara bila hata wenyewe kujua.
Kwa bahati mbaya sana, wanawake wanaoathirika zaidi na mtindo huu, ni walioolewa toka katika makabila mengine yasiyofanya ukatili huu.
Ni wazi ni ukatili kwa sababu unapomfanyia ukeketaji mwanamke wakati wa kujifungua tena bila yeye kujijua, huwa katika maumivu ya kuathirika kwa tohara pamoja na uzazi (Double effects).
Hivi ndugu zangu Wakurya na makabila mengine katika jamii zote za ki-Afrika, kinachowahangaisha ni nini na kina faida gani? Hivi kweli kitendo hicho ni spidi gavana ya ufuska? Ni ufahari? Mbona nanihii amefanya lakini ….. tandiko la kukodi? Au….. mbona nani hii hajafanyiwa lakini; ni mtu mtii wa maadili?
JULAI,1998 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya makosa ya kujamiiana ikaweka adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa anaepatikana na kosa la kubaka, kunajisi ama kulawiti.
Sheria hiyo pia inambana mtu anayepatikana na hatia ya kuhusika na kukeketa kwa namna yoyote ile, ambapo adhabu yake ni kifungo miaka mitano jela.
Pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo, vitendo vya ukeketaji na ubakaji bado vinazidi kushamiri badala ya kupungua tangu kupitishwa kwa sheria hiyo.
Kwa upande wa ukeketaji wa wanawake, hivi sasa wadau mbalimbali hapa nchini wamejitokeza kupambana na mila hii potofu ambapo hutoa elimu juu ya madhara ya mila hii.
Hata hivyo, pengine ni vizuri kwanza tukaelewa zaidi kuwa mtu anaposema ukeketaji ; anakuwa na maana gani.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ukeketaji ni kitendo cha kushona au kukata kipande au kuondoa sehemu ya juu ya siri ya mwanamke kwa sababu yoyote ile (tohara kwa wanawake).
Utafiti umebainisha kuwa hali hiyo huleta madhara ya muda mrefu kwa wale wanaotendewa kitendo hicho.
Takwimu kuhusu idadi ya wanawake wanaofanyiwa tohara hii katika Tanzania inasemekana kuwa kwa hivi sasa ni zaidi ya asilimia 18, na kwa inakisiwa kwamba zaidi ya wanawake milioni 130 hufanyiwa ukeketaji kila mwaka duniani.
Mojawapo wa Wadau hao ni Kanisa Katoliki kupitia kitengo chake Maedendeleo ya Akinamama kilichopo chini ya Shirika la Misaada,CARITAS tawi la Tanzania (WID).
Kitengo hicho kimeandaa mpango wa miaka 3 wa kuelimisha umma madhara yatokanayo na ukeketwaji wa mwanamke.
Madhumuni ya mpango huo ni kuwakutanisha watu wa aina mbalimbali ili kuwaelimsha madhara ya mila hii ili kuwezesha kupata njia mbadala ya kuweza kuitokomeza.
Mratibu wa WID kitaifa,Bibi Oliver Kinabo, anasema Kitengo chake kama chombo cha Kanisa kimeamua kupambana na mila ya ukeketaji kwa kutambua madhara makubwa ayapatayo mwanamke aliyekeketwa.
Mpango huo unawashirikisha wananchi katika kubuni mbinu zinazofaa katika kutokomeza mila ya ukeketaji wanawake .
Bibi Kinabo anasema mpango huu umebuniwa baada ya kuona mila hii ya kukeketa wanawake haikomi na badala yake, inashamiri hususan katika Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania, Kanda ya Kati, ambayo ni Dodoma na Singida.
Kwa mujibu wa Bibi Kinabo, Mikoa mingine ambayo inaongoza kwa mila hii kwa hivi sasa ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Mara na Manyara.
“Mpango huu wa kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji ambao utadumu kwa muda wa miaka mitatu mfululizo, tumeupanga kimajimbo, na kwa kuanzia tumeanza na Dayosisi ya Musoma, Arusha, Same pamoja na Mbulu”. Alisema Bibi Kinabo.
Anasema Kanisa linapambana na ukeketaji ili kukomesha ukatili wa kijinsia ambao pia, unachangia maambukizi ya virus vya HIV vinavyosababisha UKIMWI.
Utafiti umebaini kuwa mara nyingi vifaa vinavyotumika katika ukeketaji si salama kiafya. Vifaa hivi ni pamoja na visu, vipande vya chupa, vyuma, nyembe na vitu vingine vyenye ncha kali.
Kibaya zaidi ni kwamba vitu hivyo hutumika mfululizo kukeketa mtu zaidi ya mmoja bila kufanyiwa usafi wa aina yoyote kama tahadhari ya kuzuia maambukizo ya virus vya maradhi mbalimbali.
Katika mpango huo wa kuelimsha jamii, WID pia, inashirikiana na kitengo kama hicho kutoka nchini Eritrea kupitia CARITAS Eritrea ambacho kinafadhili mpango huo katika Jimbo la Mbulu.
Utafiti zaidi umebaini kuwa baada ya Serikali kupiga vita suala, hivi sasa wahusika wamebaini mtindo wa kuwakeketa watoto wadogo kwa madai kuwa ni kuondoa fedheha katika familia.
Ni jambo la wazi kuwa huu nu ukatili wa kutisha.
Kulingana na utafiti huo uliofanywa na WID, baadhi ya makabila yanafanya ukeketaji kama njia ya kumwingiza msichana katika utu uzima.
Jamii nyingi nchini zimeonesha kuwa tohara hii inasisitizwa na vijana wenyewe wanaodhani kwamba kama hawatakeketwa hawatakubalika katika jamii hizo.
Bibi Kinabo anatoa wito kwa wahanga wa vitendo hivyo, kuwa mstari wa mbele kuvikemea na kuielimisha jamii kwa kuwa wanajua madhara yake.
“Sisi kama Kanisa hatukatai mila na desturi za makabila mbalimbali ambazo zinatumika kwa hivi sasa, lakini hatuko tayari kabisa kuona mwanamke akidhalilishwa kwa kukeketwa na kufa kwa mateso makali pasipokuwa na hatia. Tutaendelea kuipiga vita mila hii mbovu,” alinasema
Katika nchi nyingi duniani imeonekana kuwa elimu ndiyo njia bora zaidi inayoweza kutumika katika kupiga vita mila ya ukeketaji.
Nchini Sierra Leone, mila ya ukeketaji imekuwapo kwa karne nyingi, lakini hivi sasa kuna majimbo 588 ambayo yanawakilisha zaidi ya watu 200,000 ambako ukeketaji umeachwa kabisa baada ya wanachi kuelimshwa na kujua madhara yake.
Cha msingi kujiuliza hapa ni kuwa, inapoelezwa kuwa kitendo cha tohara kwa mwanamke (ukeketaji) kinapunguza tamaa na hisia za kawaida za kimwili, maana yake ni nini; kwamba jamii zinazofanya vitendo hivyo huwa zinalenga kuwatia vilema wanawake au kuwafanya tasa au vipi?
Kwa nini jamii ilazimishe kuwapa watu wake vilema vya uzazi? Hivi unamuondelea mtu tamaa ya mwili ili afanye nini kupata watoto ndani ya ndoa yake halali ya kidini, kiserikali na hata kijamii? Tena ikumbukwe kuwa hiyo ni ndoa ile mnayosherehekea huku mkila na kunywa kwa mbwembwe.
Nina wasiwasi kuwa Serikali na jami yenyewe wakiwamo Wakurya visiposhirikiana kuupiga vita unyama huu, utafikia wakati utakuwa ni utaratibu kabisa kuwa watoto wa kike watahiriwe wakiwa wachanga tena wakati ule wanapozaliwa. Mateso, aibu na unyama tupu.
Hivyo, nguvu za pamoja zinahitajika sana kukemea vitendo hivi viovu.
Mara nyingi Wakurya wenyewe wameshuhudia namna vifo vanavyotokea wakati wa kujifungua kutokana na tohara hizo haramu, namna wanavyovuja damu baada ya kitendo hicho. Ni nani asiyejua tabu na maumivu makali wanayoyapata wanawake wanapotolewa damu ile inayotokana na tohara (amakoha)?
Nani hajui namna wengine wanavyozimia huku wakipiga mayowe ya vilio vya uchungu? Ndani ya mateso hayo ambayo wengine huyashangilia kwa kula na kunywa huku mwingine akinusurika au kufa?
Hivi ni mzazi gani mwenye busara anayefurahia kumjeruhi mwanae kwa makusudi huku yeye akila na kunywa kwa furaha hali anajua hakuna faida yoyote bali hasara tupu? Hivi Wakurya kuna nini wanachong’ang’ania . Kilicho cha maana ni kipi chenye faida katika suala hilo la tohara kwa wanawake?
Umefika wakati jamii ya Wakurya sasa ijiulize inatoka wapi, na inakwenda wapi. Jamii haina budi kuzitazama upya mila na desturi.
Zipo nyingine ambazo hazina budi kuigwa na kurithishwa toka kizazi kimoja hata kingine kama zile za kushirikiana katika kazi kama kilimo, ujenzi, ulinzi na usalama, kusaidiana wakati wa maafa na mengine ya namna hiyo.
Hawana budi kuzitambua haki za watoto wote; wa kike na wa kiume na kuwapa huduma za jamii kama elimu na afya.
Wajue kuwa dhana ya kuwatahiri watoto wa kike kwa kificho na wakati wa kujifungua ni sawa ujanja wa popo kutaka kumnyea Mungu kumbe anajinyea mwenyewe.
Jamii ijue kuwa njia za kumuangalisha mtoto wa kike zipo nyingi na hata kwa vipindi vingi tofauti.
Hizo zinawezekana hata bila ya kufayika tohara. Kwani makabila yasiyo na tohara kwa watoto wa kike hawana maadili?
Inabidi sasa Wakurya na Watanzania kwa jumla, waijenge jamii yao kijamii na kiafya; siyo kuzidi kujimaliza na kujibomoa wenyewe kutokana na mila na desturi zilizopitwa na wakati; tena zisizo na faida.
Ni kutokana na athari za tohara kwa wanawake ndiyo maana labda hatutakosea kusema kuwa nakabila yanayofanya hivyo wakiwamo Wakurya, pamoja na mengine yooote mazuri; lakini hili linawaharibia hadhi, afya na jamii yao, achilia mbali suala la ugomvi wa ovyo ovyo. Hata hivyo, inafurahisha kuona walio wengi sasa wanabadilika na kw
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment