Monday, December 17, 2012

Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki?

Na Cosmas J.Pahalah Katika Toleo lililopita, Askofu Method Kilaini, aliishia katika kusema kuwa, kwa bahati mbaya, kwa kuwa walioanza walikuwa Walokole, utakuta mara nyingine katika Uamsho wa Kikatoliki Walokole utakuta pia wamo humo na hata wanajaribu kuleta vitu vyao vya Ulokole humo ndani. Endelea. Kwa maana hiyo, Uamsho unakuwa ni kitu ambacho badala ya kuwa na vya kufundisha, unakuta unabakia tu ni kitu cha kuimba, kusema lugha na na katika kujaribu kuponya vyote unakuta vinabaki hapo. Uamsho unabaki ni hapohapo ambapo unakuwa kama vile hauna maana. Uamsho ni kitu kikubwa zaidi. Ni katika kujaribu kuingiza dini katika mtu ili aweze kumuamini Kristo katika roho inayosema, hauwezi kusema Kristo ni Bwana bila nguvu ya Roho Mtakatifu. Hiki ndicho kiini chake; kusema kwamba Kristo ni Bwana kwa nguvu za Roho Mtakatifu, hivyo vitu vingine vya lugha, kuponya, kuimba na kurukaruka ni vitu vya kusaidia, wala siyo kiini cha Uamsho. Hivyo, utakuta kosa linalofanyika mara nyingine ni kufanya hivyo kama ndiyo kiini cha Uamsho na hoja inakuwa ni Uamsho. wanapoimba na kuruka, inakuwa Uamsho wanaponena kwa lugha, unakuwa Uamsho wanapoponya, hivyo inaendelea hata kufikia kwamba pengine watu wasiende hospitali tena. Hivyo, pengine unaambiwa nenda kwa Wanauamsho utaponywa. Kwa hali kama hiyo, mtabakia kila wakati mnawahubiria watu kuwa wakienda kwenye Ulokole, wanaenda kupona. Ukweli siyo huo. Hata Kristo mwenyewe hakuponya kila mtu, ila kuponya ilikuwa ni ishara ya ujumbe alioutoa. Hiki ni kitu kimojawapo ambacho Uamsho kama unataka kufanikiwa, unapaswa kujihadhari nacho. Uamsho tunauita Uinjilishaji wa Kina, ili watu waseme Kristo ni Bwana, na hivyo wabadili maisha yao. Ndiyo maana Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alianzisha Kituo cha Agape (Agape Center). Kwa kweli kilikuwa Kituo cha kwenda kuandaa watu na kuwafanya kuwa wainjilishaji wenye moyo na dhamira kubwa ya kwenda kufundisha na kuleta uinjilishaji wa kina. Na hii ndiyo iliyokuwa dhamira kuu ya Mkutano wa AMECEA wa Mwaka huu. Hivyo, wanapokwenda waingie katika parokia wakiwa wanyenyekevu. Na jambo tunalowaomba mapadre ni kuwa karibu nao. Hii itasaidia kuwafanya wasiiache iende peke yake. Pia, wasiseme hawaijui. Wajaribu kuielewa kwa sababu ni sehemu mojawapo ya karama za Bwana. Nilikwenda katika parokia moja, nikakuta Kamati Tendaji, tukaongea. Lakini, mmoja akasema eti kama angekuwa na uwezo, angefuta hii Karismatiki eti ili Kanisa liwe na amani. Nikasema hapana, hatuwezi kufuta Uamsho. Uamsho upo. Hata ukiwafukuza katika parokia yako, au katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, bado Nairobi watafanya, Kampala watafanya; na wale wa Nairobi watakuja huku, sijui sasa tuwafukuze kanisani! Kuwafukuza kanisani sio suluhisho, suluhisho ni kuwaelewa na kuwasaidia kulijenga Kanisa. Ukiwafukuza katika parokia, haimaanishi kuwa Wakristo wako wakiwa Wanauamsho, utawakatalia sakramenti. Huwezi. Watakwenda katika parokia nyingine, watakuwa Wanauamsho watarudi na kufanya chinichini na hii itaharibu uchungaji. Mfano, katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, tunaweza kusema tunafuta Uamsho, lakini wakatoka kwingine mfano, Morogoro, Arusha, Mbeya, Nairobi; watakuja, wataingia na huwezi kuwakataza wala kuwasimamisha sakramenti kwa sababu eti umepiga marufuku Uamsho. Uamsho ni kitu halali hata toka Roma, hivyo suluhu ni kuukubali, kuishika na kuilea Karismatiki ili iendelee vizuri. Kuhusu karama za uponyaji, huu ni msisitizo wa Roho Mtakatifu. Unapokuwa na karama za Moyo Mtakatifu wa Yesu, hapo huwa una msisitizo tu, wa moyo mwanana wa Bwana Yesu na huruma yake. Mfano, Lejio Maria msisitizo wake ni ibada kwa Bikira Maria kama Mama, lakini Karismatiki msisitizo wake ni kujua nafasi ya Roho Mtakatifu katika imani yetu; ile ya kwenda na kuhubiri. Yaani hapa kila mtu aseme, “Ole wangu nisipohubiri Neno la Mungu.” Haya mambo mengine ya kunena kwa lugha, mambo ya kuimba, ni namna tu, za kusaidia. Ni muhimu pia watu wajue kuwa wasipopona, wasiseme kuwa Roho Mtakatifu hayupo, vinginevyo wagonjwa wote tungewatoa hospitali ili waende pale wakapone. Lazima watu wajue kuwa Mungu akipenda, anaweza kumponya hata mtu mmoja tu. Na hii nasema sio kwa Karismatiki peke yake, hata kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu; wanaweza kuombea mtu, Mungu akipenda, anapona, Lakini hakuna anayeweza kusema eti mimi kama Mkarismatiki nasema kuwa pona na hivyo eti mtu yule naye apone. Hapa ni Mungu ndiye anayeponya na sio Mkarismatiki na wala sio dini. Karama za Karismatiki ni kueleza Neno la Mungu; kuinjilisha kwa kina. Itaendelea

No comments:

Post a Comment